Saturday, February 21, 2015

Mwanamke Amkata Mpwa Wake Sehemu za Siri Huko Ruvuma

Mtu mmoja wa Kijiji cha Majimaji Ruvuma, Patrick Vitus amekatwa sehemu zake za siri  na kuachwa zikining’inia. 

Ofisa Mtendaji Wa Kijiji hicho Hussein Mkali amesema Partick alikatwa sehemu zake za siri na mpwa wake Zainabu Saidi baada ya kumkatalia kwenda kumfuata mume wake anayeitwa Musa Said ambaye alikuwa kwa mke mdogo.
 
Baada ya kufanya tukio hilo Ofisi ya Kijiji ilimkamata Zainabu na kumpeleka katika kituo cha Polisi, huku Patrick akipelekwa Hospitali ya Tunduru kwa ajili ya matibabu.

http://www.mpekuzihuru.com/2015/02/mwanamke-amkata-mpwa-wake-sehemu-za.html

Friday, February 20, 2015

Mkuu wa Kituo cha Polisi Ilembula Njombe Afungwa Jela Miaka 30 kwa kosa la Kumbaka Mahabusu

Mahakama ya Hakimu Mkazi Mkoa ya Njombe, imemhukumu aliyekuwa mkuu wa kituo cha Polisi Ilembula kifungo cha miaka 30 jela, baada ya kukutwa na hatia ya kumbaka  mtuhumiwa aliyekuwa ndani ya mahabusu. 

Hukumu hiyo ilitolewa na Hakimu Augustine Rwezile, baada ya mshtakiwa huyo James Nyambenga kukiri kosa hilo mahakamani, ambapo mshakiwa huyo anadaiwa kumtoa msichana huyo kwenye chumba cha mahabusu alikokuwa anashikiliwa na kumbaka.
 
Mwanamke huyo ambae ni mhudumu wa bar alikuwa anashikiliwa kwenye mahabusu ya kituo hicho kwa tuhuma za uzururaji.
 
Akisoma hukumu hiyo Hakimu Rwezile amesema ushahidi uliotolewa na upande wa mlalamikaji na vielelezo vya daktari aliyempima msichana huyo viliweza kuithibitishia Mahakama kuwa mtuhumiwa alitenda kosa hilo.

chanzo:http://www.mpekuzihuru.com/2015/02/mkuu-wa-kituo-cha-polisi-ilembula.html

Wednesday, February 18, 2015

JWTZ wajaribu kumkomboa mwanajeshi aliefungwa. Ni mtoto wa muasisi wa Mapinduzi Z’bar

Baada ya kuhukumiwa kutumikia gerezani kwa muda wa siku 15  kila mmoja kwa watoto sita wa muasisi wa Mapinduzi ya Zanzibar, marehemu Khamis Daruweshi, askari wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) jana walifika Mahakama Kuu Vuga, kuomba mmoja ya wafungwa hao ambae ni mtumishi wa jeshi, aruhusiwe akatumikie adhabu mahabusu ya jeshi.


Zanzibar Leo iliwashuhudia askari wa jeshi hilo zaidi ya 10, wakiingia mahakamani na kufanya mazungumzo na Mrajisi wa mahakama, George Kazi, ambae ndie alietoa adhabu hiyo.

Mtumishi huyo wa jeshi aliehukumiwa kifungo kwa kosa la kudharau amri ya mahakama pamoja na wenzake watano ni Darwesh Khamish Darwesh.

Juzi Mrajisi huyo ambae pia ni Hakimu wa mahakama ya Mkoa, aliwatia hatiani watoto hao sita wa familia moja kutumikia Chuo cha Mafunzo kwa muda wa siku 15 kila mmoja kwa kosa la kudharau amri halali ya mahakama.

Wadaiwa wengine katika shauri hilo ni Shaabani, Said, Asia, Atinji pamoja na Atika ambao wote hao ni watoto wa marehemu Khamis Darwesh, ambao inadaiwa walikataa amri halali ya mahakama ya kutakiwa kuhama katika nyumba yao inayobishaniwa baada ya mahakama kutoa maamuzi ya kuuzwa.


Hata hivyo, Mrajisi huyo aliwakatalia wanajeshi hao kumchukua mwanajeshi mwenzao kwenda kutumikia adhabu jeshini, akisema uamuzi huo umefanywa kwa mujibu wa sheria.

Aidha aliwambia  wanajeshi hao kuwa wana nafasi ya kuwasilisha ombi la mapitio ya shauri hilo mahakama kuu ili liweze kusikilizwa.

Baada ya kauli hiyo, wanajeshi hao waliondoka katika maeneo ya mahakama.

Habari za uhakika zilizopatikana baadae jana zinasema baada ya zoezi la kumuomba Mrajisi kumuachia mwanajeshi huyo, askari wengine wawili wa JWTZ walifika ofisini kwa Jaji Mkuu wa Zanzibar, Omar Othman Makungu, kwa kile kilichoelezwa kutafuta njia ya kumnasua mwanajeshi mwenzao.

Mwanajeshi huyo na wenzake walikumbwa na mkasa huo baada ya kushindwa kuielezea mahakama sababu iliyowafanya washindwe kuhama ndani ya nyumba iliyoachwa na marehemu baba yao Khamis Darwesh iliyouzwa kwa amri ya mahakama.

Nyumba hiyo iliyopo Kilimani Kiungani plot namba 15, 17 na 18 iliuzwa na kampuni ya mnada ya Kumekucha kwa idhini ya mahakama baada ya kufunguliwa kesi ya madai iliyohusisha familia ya marehemu.


Mara baada ya nyumba hiyo kuuzwa, kampuni ya Kumekucha iliwaandikia barua wakaazi wa nyumba hiyo kuhama ili akabidhiwe mmiliki halali  aliyeinunua lakini familia hiyo ilikataa wakidai nyumba hiyo marehemu baba yao ambao aliiweka wakfu.

chanzo:zanzinews

Tuesday, February 10, 2015

Babu Amlawiti Mjukuu Wake wa Kike.....Amhonga sh.2000 ili Asitoe Siri

POLISI wilayani Masasi mkoani Mtwara inamshikilia mkazi wa kijiji cha Maili Sita kata ya Mtandi, Daudi Pilipili (44) kwa tuhuma za kumlawiti mjukuu wake wa kike mwenye umri wa 13.

Mkuu wa Polisi wilaya ya Masasi, Azaria Makubi alisema inadaiwa alitenda kosa hilo juzi saa 9:00 katika kijiji cha Maili Sita huku bibi wa mtoto akiwa amekwenda nyumbani kwa mwalimu wa shule anakosoma mjukuu wake (aliyelawitiwa) kwa mazungumzo.
 
Alisema siku ya tukio mzee huyo alimkamata mjukuu wake na kumwingiza chooni huku akimweka vitambaa mdomoni asitoe sauti na alipomaliza kitendo chake hicho cha kinyama alimpatia mtoto Sh 2,000 ili asitoe siri kwa wazazi wake.
 
Inadaiwa watoto wenzake ndio waliotoa taarifa hiyo baada ya kushuhudia kitendo hicho kikifanyika na polisi kutaarifiwa.

http://www.mpekuzihuru.com/2015/02/babu-amlawiti-mjukuu-wake-wa.html

Afisa Mtendaji Atandikwa Makofi Hadharani

OFISA Mtendaji wa kijiji cha Lumesule, Kata ya Lumesule, wilaya ya Nanyumbu mkoani Mtwara, Swalehe Daimu, anadaiwa kupigwa na mkazi wa kijiji hicho, kwa madai ya kumkamata dada yake na kumtoza faini ya Sh 5,000 kwa kushindwa kushiriki shughuli za ujenzi wa maabara.
 
Akizungumza mbele ya Mkuu wa Mkoa wa Mtwara Halima Dendegu, kijijini hapo jana, mlinzi huyo wa amani alisema kuwa tukio hilo limetokea Februari 4 mwaka huu, baada ya kuwakamata watu kumi kijijini hapo ambao hawakushiriki katika ujenzi wa maabara zinazoendelea kujengwa katika shule ya sekondari Lumesule.
 
“Sisi kama kijiji tumetunga sheria ndogo za usimamizi wa ujenzi huu, na mwananchi yeyote ambaye hakushiriki ni lazima akamatwe na kisha atozwe kiasi hicho cha fedha ili zisaidie kuendeleza ujenzi,” alisema.
 
”Baada ya kuwa nimewashikilia hawa watu na kuwafungia katika ghala la kijiji, huyo bwana alikuja kwa ajili ya kumlipia ndugu yake faini hiyo na kisha kunipiga vibao na kisha kunitishia maisha,” alifafanua Daimu.
 
Kwa mujibu wa mtendaji huyo, mtuhumiwa huyo amekuwa kikwazo kikubwa kwa shughuli za maendeleo kijijini hapo kwa kuwashawishi wananchi kutoshiriki shughuli za ujenzi wa maabara na miradi mingine ya maendeleo.
 
Akieleza tukio hilo, Daimu alilitupia lawama Jeshi la Polisi kwa kushindwa kumkamata mtuhumiwa licha ya kutoa taarifa kituo kikuu cha Polisi cha wilaya Mangaka, na kwamba mpaka sasa mtuhumiwa huyo yupo kijijini hapo , anaendelea kuwashawishi wananchi kukataa kushiriki ujenzi huo.
 
Kutokana na hatua hiyo Mkuu wa Mkoa wa Mtwara Halima Dendego, ambaye yupo ziara ya ukaguzi wa maabara katika wilaya hiyo, alimwagiza Mkuu wa wa Wilaya kukamatwa haraka kwa mtuhumiwa huyo na kumfikisha mahakamani.

http://www.mpekuzihuru.com/2015/02/afisa-mtendaji-atandikwa-makofi.html

Monday, February 9, 2015

Baba Amuunguza Mdomo Mwanae kisa Kadokoa Maharage

Vitendo vya kikatili na unyanyasaji wa Wanawake na watoto vinaendelea kushika kasi licha ya Serikali na mashirika mbalimbali ya haki za Binadamu kupiga vita vitendo hivyo kwa nguvu .

Hali hiyo imejitokeza katika kijiji cha Kasaka, Kata ya Nyaruyoba Wilaya ya Kibondo mkoani Kigoma baada ya Baba mzazi aliyefahamika kwa jina la Sindotuma Nyamubi, kumchoma moto na kumuunguza vibaya sehemu za mdomoni wake, mtoto wake wa miaka saba akimtuhumu kudokoa maharage yaliyotakiwa kutumika kama mboga kwa ajili ya kulia chakula.

Afisa Mtendaji wa kijiji hicho Bwa Felix Cosmas amesema kuwa mtoto huyo alibainika kuwa amefanyiwa kitendo hicho baada ya majirani kutomuoana akicheza na wenzake kwa muda wa siku tatu kama ilivyokuwa imezoeleka, ndipo walipogundua alikuwa amefichwa ndani ya nyumba na kugundua tatizo hilo na kutoa taarifa hatua iliyofanikisha mzazi huyo kukamatwa na kufikishwa Polisi.

Naye Afisa Ustawi wa Jamii wilaya ya Kibondo,Bi Sofia Gwamagobe amesema kuwa ni vizuri wazazi na walezi kutambua na kujali hali za watoto na sambamba na jamii pia kuendelea kufichua na kutoa taarifa katika vyombo husika ili kuweza kuokoa maisha ya watu wanaofanyiwa mambo kama hayo kama wamejeruhika kuwapatia matibabu kabla hawajapata madhara makubwa

Mkuu wa Jeshi la Polisi wilayani Kibondo, amekiri kuwepo kwa tukio hilo, na kumtaja aliyejeruhiwa vibaya kuwa ni Shukuru Sindotuma na amesema baada ya mtuhumiwa huyo kufikishwa kituoni hapo, amekubali kuwa alimchoma moto mtoto wake kwa kosa la kula maharage bila ruhusa yake

Mtoto huyo Shukuru Sindotuma alikuwa anaishi na baba yake ,mdogo wake mmoja huku Wazazi wao wakiwa wametengana.

chanzo:http://www.mpekuzihuru.com/2015/02/baba-amuunguza-mdomo-mwanae-kisa.html

Thursday, February 5, 2015

Mtuhumiwa Aua Polisi Kwa Panga Dodoma

Polisi mkoani Dodoma wanamsaka mkazi wa Chang’ombe Juu, Tisi Malya kwa kumuua askari polisi kwa kumcharanga mapanga wakati akijaribu kumuokoa mtoto wa miezi minane aliyekuwa anataka kuuawa na mtu huyo.

Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Dodoma, David Misime amemtaja askari aliyeuawa majira ya saa 5:00 asubuhi kuwa ni Joseph Swai.
 
Akisimulia mkasa huo kwa waandishi wa habari, Kamanda Misime alisema kuwa askari huyo aliitikia mwito uliofika kwake wa kuwepo kwa dalili ya tendo la jinai nyumbani kwa mkazi mmoja wa Chang’ombe Juu katika Manispaa ya Dodoma.
 
Alisema askari huyo alipigiwa simu na Mtendaji wa Mtaa wa Chang'ombe Juu, akimjulisha kuwa amepokea taarifa ofisini kwake kutoka kwa Oliver Baltazar(52) mkazi wa Chang'ombe Juu kuwa mtoto wake, Tisi Sirili anaonekana anataka kumuua au ameshamuua mtoto wake wa miezi minane, Valerian Tisi.
 
Alisema baada ya kupokea taarifa hiyo, askari huyo alikwenda ofisini kwa mtendaji huyo ambapo waliongozana hadi nyumbani kwa mtuhumiwa.
 
"Alipofika askari aligonga mlango huku akijitambulisha kuwa yeye ni askari ili mtuhumiwa atoke nje, alichofanya mtuhumiwa ni kumnyanyua mtoto wake mdogo wa miezi minane kwa mkono mmoja kichwa chini miguu juu na kutaka kumkata kwa panga huku akisema, ‘namkata shingo na sitaki kuona mtu’.
 
"Askari aliamua kumwokoa mtoto huyo kwa kumrukia mtuhumiwa, lakini kwa bahati mbaya aliteleza na ndipo mtuhumiwa akamkata kichwani askari wetu," alisema Misime.
 
Alisema pamoja na askari huyo kuanguka, mtuhumiwa aliendelea kumkatakata kwa panga huku mtendaji na kijana waliyekwenda naye eneo la tukio, wakikimbia huku wakipiga kelele za kuomba msaada.
 
Alisema mtuhumiwa baada ya kufanya kitendo hicho cha kinyama, alikimbia akiwa na panga lake huku nguo zake zikiwa zimetapakaa damu.
 
Aidha, alisema katika hekaheka hizo, mama wa mtoto baada ya kuona mtoto amebwagwa na askari ameanguka  chini, naye alimkwapua mtoto na kukimbia naye mahali pasipojulikana. Alisema polisi wanamsaka  baba huyo na mama huyo  kwa ajili ya usalama wake.

http://www.mpekuzihuru.com/2015/02/mtuhumiwa-aua-polisi-kwa-panga-dodoma.html